Monday, 12 May 2014

WANAFUNZI WA MASASI GIRLS - MTWARA WAANDAMANA KUPINGA KIFO CHA MWANAFUNZI MWENZAO KILICHOSABABISHWA NA UZEMBE WA MWALIMU MKUU

Wanafunzi  wapatao 344 wa shule ya sekondari ya wasichana Masasi mkoani Mtwara wameandamana hadi nyumbani kwa Mkuu wa wilaya ya Masasi, Farida Mgomi wakishinikiza  kuondolewa kwa mkuu wa shule hiyo, Reinader Tesha kufuatia kifo cha mwanafunzi mwenzao wa kidato cha tano Omega Kabuje aliyefariki jana (Jumamosi), FikraPevu imeelezwa.
Wakati wanafunzi hao wakiwa katika maandamano ambayo yaliyofanyika leo(jumapili) kuanzia saa 11 alfajiri ambayo hata hivyo hawakufanikiwa kukutana na mkuu wa wilaya, Mgomi kwani alikuwa safarini Mtwara, mkuu  wa shule hiyo ya wasichana Reinader Tesha alijikuta akipoteza fahamu na kukimbizwa hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Masasi ya Mkomaindo ambapo anaendelea kupata matibabu baada ya kuanguka ghafla akiwa nyumbani kwake baada ya kujifungia kwa takribani saa nne.
Hatua ya wanafunzi hao ambayo imekuja wakati tume iliyoundwa na baraza la madiwani kuchunguza malalamiko yanayomhusu mkuu wa shule hiyo jinsi anavyowanyanyasa wananfunzi wake na utendaji wake wa kazi hasa tuhuma za manyanyaso yanyofanyiwa wanafunzi wa shule hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Dada mkuu wa shule hiyo, Regina Christopher alibainisha kuwa wamechukua hatua hiyo baada ya kuchoshwa na vitendo vya mkuu huyo ambapo mara zote amekuwa anawanyanyasa na kutowathamini pindi wanapokuwa wagonjwa na walimu wa kutowajali wanafunzi.
Alidai kuwa mkuu huyo wa shule amekuwa hafuatilii wanapougua ambapo jukumu linakuwa la wanafunzi wenyewe kutafuta usafiri wa kuwapeleka hospitali kwa ajili ya kupata matibabu kwani shule haijishughulishi na huduma za matibabu.
“Mwenzetu amefariki leo na hii tunajua si kwa mipango ya Mungu bali kuna uzembe wa walimu na watoa huduma hivyo tumeamua leo kuandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya kuonesha kukerwa na tabia hizo,” alisema Regina.
Kiongozi huyo wa shule pia alilalalamikia huduma mbovu inatolewana wahudumu wa hospitali ya wilaya wananfunzi hao wanapofika kupata huduma za matibabu ambapo wahudumu hao huwa wanawatolea maneno ya dharau na kejeli hali ambayo pia inaweza kuwa ilichangia kifo cha mwanafunzi mwenzao.
Akizungumzia tukio hilo Makamu mkuu wa shule hiyo, Vestina Nditi alikiri kutokea mgogoro huo na kuwa ulitokana baada ya mwanafunzi wa kidato cha tano Omega Kabuje kufariki akiwa hospitali.
Hata hivyo, alisema ya kuwa malalamikio yaliyotolewa na wanafunzi si ya kweli kwani uongozi wa shule unajitahidi kuwapatia huduma mbalimbali wanapokuwa wagonjwa na kuwa tatizo kwa sasa shule hiyo haina  mlezi ambaye ana taaluma ya uuguzi.
“Hizo taarifa si sahihi kwani kwa uwezo wetu walimu tunajitahidi kuwahudumia wanafunzi ila tatizo shule kwa sasa haina mlezi mwenye taaluma ya uuguzi ingawa tumeahidiwa na halmashauri kuwa tutampata hivi karibuni,” alisema Nditi.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Masasi, Dkt Harry Mwambe alikiri hospitali yake kumpokea mwanafunzi huyo siku ya ijumaa saa kumi na moja jioni ambapo baada ya uchunguzi wa vipimo vya kitabibu alibainika kuwa alikuwa na malaria kali na jana (Jumamosi) saa 10.15 alifariki dunia.
Akizungumzia malalamiko yaliyotolewa na wananfunzi hao, Mganga mkuu huyo alisema kuwa hana taarifa juu ya malalamiko hayo na kuwa atayashulikia na kama ikibainika yana ukweli atachukua hatua kali kwa wale wenye tabia hizo

No comments: